Kubenea afunguka, ni baada ya gazeti lake la Mwanahalisi kufungiwa
Kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) inayomiliki magazeti ya Mwanahalisi, Mawio na Mseto imesema itafungua kesi mahakamani endapo Serikali haitaondoa zuio la kulifungia kwa miaka miwili Mwanahalisi.
Kampuni hiyo imesema endapo leo na kesho Serikali haitalifungulia gazeti hilo watafungua kesi na kuiomba Mahakama ifute zuio hilo na kudai fidia ya Sh41 milioni kwa kila chapisho tangu zuio lilipoanza kutekelezwa.
Septemba 19, Serikali ilitangaza kulifungia gazeti hilo ikisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na mfululizo wa matukio ya ukiukwaji wa misingi na sheria za taaluma ya uandishi wa habari, kuandika habari za uchochezi na kuhatarisha usalama wa Taifa.
Mhariri Mtendaji wa Mwanahalisi, Saed Kubenea leo Jumatano katika mkutano na waandishi wa habari amesema gazeti hilo kwa miaka 12 tangu lianzishwe haliandiki upotoshaji bali ukweli.
Kubenea ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo amesema kufungiwa kwa magazeti ya kampuni hiyo ni uonevu licha ya kukiri baadhi ya maonyo waliyopewa na Serikali.
Kubenea amesema habari zilizotumika kulifungia gazeti hilo ni za ukweli.
No comments