Mapya Yaibuka Sakata la RC Makonda na Meya Jacob
Suala la Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, limechukua sura mpya baada ya meya huyo kuitwa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma na kutakiwa kujibu shauri lililofunguliwa la matumizi ya ofisi ya umma kwa shughuli za chama chake.
Machi 22, mwaka huu Meya Jacob aliwasilisha mashitaka dhidi ya Makonda kwa Sekretarieti hiyo, akitaka achukuliwe hatua za nidhamu kwa kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kutumia vyeti feki na hivyo kukosa sifa ya kuwa kiongozi.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka katika mahojiano na sekretarieti hiyo jana, Jacob alisema sekretarieti hiyo imemwomba kujibu shauri hilo ikisema kwa kuwa hata yeye aliwahi kutumia Ofisi za Manispaa ya Ubungo kwa vikao vya chama chake.
“Wameniomba kuondoa shauri hili kwa madai kuwa walipomwita Makonda alisema tuyamalize kwa kuwa hata mimi nilitumia ofisi ya umma kufanya vikao vya chama… mimi nimesema ruksa kunihukumu kama wana ushahidi wa kutosha,” alisema Jacob.
Alisema uhalali wa Makonda kumhoji kuhusu kufanya vikao vya chama katika ofisi ua umma ndiyo mwanzo wa uhalali wa kumhoji mkuu wa nchi uhalali wa kufanya vikao vya chama Ikulu.
“Hakuna kikao ambacho nilikiongoza mimi nikiwa na wafuasi wa chama, ninachojua nilitembelewa na Frederick Sumaye. Kiongozi wa Chadema akinitembelea nimkatae? “Lakini wenzetu wamefika mbali kwa kuvaa sare za chama na kuzungumza masuala ya chama,” alisema.
Alisema wanaporuhusu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kumuuliza kuhusu hilo walipaswa waanze kujitafakari kuwa kuna Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inafanyika Ikulu.
Alisema walimwambia hakuna mtu aliyewahi kulalamika kwa nini mikutano ya CCM inafanyika Ikulu.
“Sheria inasema wao waliposikia tu kuwa Makonda ana vyeti feki walitakiwa kumwita na si kusubiri mtu aende kushtaki.
“Wao kama wasimamizi wa maadili ya umma wakiona mtu anarudisha fedha za rushwa benki hawakustahili kusubiri mtu wa Chadema kwenda kushtaki,” alisema Jacob.
Jacob alisema alipewa dakika 10 za kuandika malalamiko kwa nini CCM inafanyia vikao vyake Ikulu.
“Nimewakabidhi ushahidi wa picha na video za vikao vya Chama cha Mapinduzi Ikulu,” alisema Jacob.
Alisema lengo lake si kulalamika kuwa CCM inafanyia vikao vyake ikulu bali suala la vyeti feki ambalo anahitaji lifikishwe katika Baraza la Maadili.
No comments