Breaking News

Ndugu 6 wa Familia Moja Wahukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa


Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa imewahukumu adhabu ya kifo watu sita ambao ni ndugu wakazi wa Kalambo baada ya kupatikana hatia ya kumuua ndugu yao.

Ndugu hao wamedaiwa kwamba walifikia uamuzi wa kumuua ndugu yao huyo kwa madai ya kwamba anajihusisha vitendo vya kishirikiana.

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumanne na Jaji Mahakama hiyo, Dk Adam Mambi baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka uliopeleka mashahidi sita ili kuthibitisha mashitaka hayo.

Waliokutwa na hatia katika shauri hilo ni Ferdinand Kamande, Peter Mpandisharo, Edes Kamande, Stephen Sikanda, Henrick Nguvumali na Anatory Kamande huku Alistid Kamande na Will broad Kamande wakiachiwa huru kwa kutokutwa na hatia.

Katika shauri hilo upande wa mashitaka uliongozwa na mawakili wa serikali ambao ni Scolastica Lugongo na Adolf Lema huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Mathias Budodi, ambapo ilidaiwa kwamba washitakiwa walitenda kosa hilo Septemba 27, mwaka 2014.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa siku ya tukio nyakati za usiku washitakiwa wakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga, nondo, mawe, majembe walivamia nyumba ya Kamande na kugonga dirisha kisha kuvunja mlango ambapo Kamande alikimbia kuelekea kusikojulikana.

Ilielezwa kwamba baada ya hapo waliichoma moto nyumba hiyo na kuteketeza kila kitu kilichokuwemo ndani kisha kuondoka zao.

Wakati nyumba hiyo ikiteketea kwa moto Kamande aliyekuwa amekimbia ili kunusuru maisha yake, alikamatwa na watu hao na kuanza kupigwa huku wakimtuhumu kuwa ni mchawi na baada ya kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake walimchoma moto na kufariki papo hapo.

Ilidaiwa kwamba  washitakiwa hao walikamatwa na polisi Oktoba 10, 2014 na baada ya kuhojiwa na polisi walikana shitaka hilo.

Awali kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa Serikali waliiomba mahakama kutoa adhabu kali iwe fundisho kwani watu wamekuwa wakichukulia sheria mkononi na kuua watu kinyume cha sheria wakiwatuhumu kuwa ni washirikina.

Akitoa adhabu hiyo Jaji wa Mahakama hiyo, Dk Mambi amesema ameridhishwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka hivyo kwa kutumia Kifungu cha Sheria ya Makosa ya Jinai Namba 196 Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo 2002 anawahukumu watu hao sita kifo kwa kunyongwa.

No comments