Breaking News

Yusuf Manji Atinga Mahakamani na Muonekano Mpya.....Polisi Wapewa Onyo


Mfanyabiashara Yusuf Manji, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, jana alitinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiwa na muonekano mwingine tofauti na wiki chache zilizopita.

Manji alionekana kuwa tofauti kwani alivaa suti nyeusi na kunyoa ndevu tofauti na siku nyingine ambako amekuwa akitinga mahakamani akiwa amevaa fulana nyeusi ya mikono mirefu na suruali ya ‘jeans’ rangi ya bluu huku akiwa na nywele pamoja na ndevu nyingi.

Mbali na kutinga akiwa ‘ametokelezea’  kwa kuvaa suti hiyo sambamba na tai shingoni na viatu vyeusi, mshtakiwa huyo pia alionekana kuwa amechangamka tofauti na siku nyingine.

Manji na wenzake watatu walifikishwa jana mahakamani hapo kwa hati ya kutolewa mahabusu kwa ajili ya kwenda kuhojiwa polisi.

Tayari, Mahakama imeruhusu Manji na wenzake kwenda kuhojiwa na polisi kuhusiana na kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili kwa lengo la kukamilisha upelelezi.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa waliomba hati ya kuwatoa washtakiwa mahabusu ili kufanyiwa mahojiano katika kesi namba 33/2017 na kwamba washtakiwa hao walikabidhiwa mikononi mwa polisi.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema aliandikiwa barua na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), akiomba washtakiwa hao waende wakahojiwe polisi.

Alisema Mahakama imekuwa ikisisitiza kesi za uhujumu uchumi zikamilishwe upelelezi ili ziweze kusikilizwa.

“Tusingeweza kukataa maombi hayo kwa sababu tutapingana na kauli yetu ya kukamilisha upelelezi. Ndiyo maana tumetoa hati ya kuwatoa mahabusu kwa ajili ya mahojiano na hii si mara ya kwanza kuwatoa washtakiwa mahabusu kwa ajili ya upelelezi,” alisema Hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi aliwataka polisi kuzingatia haki za washtakiwa kwa kuhakikisha wanakuwa na afya njema na wapate uhuru wa kuwakilishwa na mawakili wao kwenye jambo lolote na isiwe kificho.

Hakimu aliwakabidhi washtakiwa hao kwa Koplo Dotto kama barua inavyoelekeza kwa kuwa Sajenti Mkombozi ambaye alitakiwa kukabidhiwa hakuwepo. Washtakiwa hao wanatakiwa kurudishwa kesho (leo) katika muda wa kazi.

Mbali na Manji, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43).

Akiwasilisha maombi hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi aliomba mahakama iruhusu washtakiwa wakabidhiwe kwa polisi ili kutimiza matakwa ya upelelezi.

Kishenyi alidai kwamba Kifungu cha 59 (1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinawapa mamlaka polisi kufanya upelelezi.

Akijibu hoja hizo, wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo alidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri kama ilivyoombwa na upande wa mashtaka kwa sababu shauri hilo halijapata hati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuipa mamlaka kusikiliza shauri hilo.

Ndusyepo alidai kuwa mahakama hiyo imefungwa mikono ya kutoa amri dhidi ya maombi hayo.

Pia alidai kifungu cha sheria kilichotajwa na upande wa mashtaka, kinazungumzia ufanyaji wa upelelezi kwa ujumla.

Wakili mwingine wa utetezi, Hajra Mungula alidai kuwa washtakiwa hao wako chini ya ulinzi na kwamba upande wa mashtaka uliwashtaki huku ukijua kwamba haujakamilisha upelelezi na umetoa hati ya kuzuia dhamana.

“Tunaomba ombi hili likataliwe na upande wa mashtaka uelekezwe kuzingatia sheria na haki za washtakiwa,” alisema Mungula.

Hata hivyo, Wakili Kishenyi alisema Mahakama imekuwa ikisisitiza kukamilisha upelelezi na kwamba wanachofanya ni sehemu ya kuukamilisha.

Pia alidai kuwa washtakiwa hao wanayo haki ya kuwakilishwa hivyo maombi yao yakubaliwe.

Hakimu Shaidi alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuwaruhusu washtakiwa hao kwenda kuhojiwa.

No comments