Zungu: Bunge Halitatunga heria ya Kuzuia Mimba Shuleni, Hilo ni Jukumu la Wazazi
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu amesema hakuna sheria itakayotungwa na chombo hicho itakayozuia mimba shuleni na kuwataka wazazi kuwajibika kutoa malezi bora kwa watoto wao ili wasipate ujauzito.
Zungu aliyasema hayo jana kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha nne katika Sekondari ya Wasichana ya Barbro Johansson akimwakilisha Spika Job Ndugai.
Alisema jukumu la kudhibiti mimba halipaswi kutegemee sheria pekee na kwamba, wazazi wanawajibika kuhakikisha wanatoa malezi bora kwa kuwa baadhi ya tabia zao zinaendana na watoto wao.
“Ukiona mtoto ni mhuni ujue na mzazi wake ni mhuni, mtoto akiwa na nidhamu na mzazi wake ana nidhamu,” alisema Zungu na kuibua gumzo miongoni mwa wazazi waliofika shuleni hapo.
“Ni jukumu la wazazi kuwalea vizuri watoto wenu na kuhakikisha hawajiingizi katika makundi hatarishi.”
Zungu ambaye pia ni mbunge wa Ilala aliwataka wanafunzi kutojihusisha na masuala ya kisiasa shuleni, bali wajikite katika masomo kwa manufaa yao.
“Kilimo ni njia ya kujikwamua kiuchumi, lakini najua vijana wengi hampendi kilimo. Niwaambieni jishughulisheni na kilimo kama sehemu ya ajira,” aliwaambia wahitimu 116 watakaohitimu.
Mbunge wa Muleba Kusini, Anna Tibaijuka alisema ni lazima jamii ikubaliane na agizo la Rais John Magufuli la kuwataka wanafunzi wanaopata mimba kutoendelea na masomo.
Tibaijuka ambaye pia ni mwenyekiti mwanzilishi wa taasisi hiyo, alisema kuwaruhusu wanafunzi wanaopata mimba kuendelea na masomo ni kuongeza tatizo .
Mkuu wa shule hiyo, Halima Kamote alisema licha ya kuwa na wanafunzi wa kike zaidi ya 600, hakuna aliyepata mimba akiwa shuleni kutokana na malezi mazuri kwa kushirikiana na wazazi.
No comments