Diamond Platnumz Kasimamsha Shughuli Hospitali Ya Amana, Jijini Dar Leo.
Mwanamuziki wa kizazi kipya Diamond Platnumz amesherehekea siku yake ya kuzaliwa leo kwa kutembelea hospitali ya Amana ambako amesababisha shughuli zisimame kwa muda.
Katika ziara yake hiyo aliyoifanya leo Jumatatu, Diamond ametoa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh4 milioni.
Muda wote aliokuwa hospitalini hapo wagonjwa na waliokuwa wakiwahudumia walitoka kwa ajili ya kumuona msanii huyo.
Diamond ambaye sasa anatamba na ngoma yake ya Hallelujah, amesema alifikia uamuzi wa kwenda kwenye hospitali hiyo kwa kuwa ndiyo mahali alipozaliwa.
Amesema anajivunia kuwa na watu wazuri wa karibu ambao wanamshauri kurudisha kwenye jamii inayomzunguka.
"Najua hospitali kuna mahitaji mengi nikaona kwa uwezo wangu mdogo nami nishiriki kusaidia mahali nilipozaliwa siku ya leo ili nipate pia fursa ya kuwaona watoto waliozaliwa tarehe kama yangu,"
"Nafahamu kuna changamoto nyingi, niwasihi watu wengine waangalie ni namna gani wanaweza kusaidia," amesema Diamond.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo, Shaany Mwaruka amempongeza Diamond kwa uamuzi huo na kutaka watu wengine waige mfano huo.
"Ungeweza kusherehekea siku yako ya kuzaliwa kwa kufanya chochote kile, lakini ukakumbuka mahali ulipozaliwa."
Dk Mwaruka amesema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba kutokana na idadi kubwa ya watu wanaowahudumia.
Kwenye ziara hiyo Diamond ameambatana na meneja wake, Said Fella.
No comments