“Usalama wa dawa nchini ni zaidi ya asilimia 95”- TFDA
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kiwango cha ubora na usalama wa dawa nchini kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 95.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo, amemweleza mwandishi wetu hivi karibuni kuwa kwa sasa usalama wa dawa nchini umeongezeka na kwamba Taasisi yake imejizatiti kuongeza weledi wa udhibiti.
“Hivi sasa udhibiti ni mkubwa hivyo dawa zetu ni salama kwa kiwango cha kati ya asilimia 92.5 hadi asilimia 98,” alisema Bw. Sillo.
Aliongeza kuwa hivi sasa hali ya soko la dawa ni salama na taasisi yake inafuatilia kwa karibu ubora na usalama wa dawa kwa kutumia mfumo maalum wa ukaguzi.
Bw. Sillo aliongeza kuwa, mafanikio hayo yanatokana na kuimarika kwa uwezo wa taasisi yake pamoja na ushirikiano mkubwa kati ya taasisi yake na wadau wakiwemo wananchi.
Mkurugenzi Mkuu huyo, alibainisha kuwa taasisi yake imeongeza uwezo wake kwa kuajiri watumishi hadi kufikia zaidi ya 300 kutoka watumishi 53 ilipoanzishwa. Aidha, mbali ya kufungua ofisi za kanda saba (07), TFDA imeongeza uwezo wa maabara zake za uchunguzi na zimepata ithibati za umahiri za kimataifa ikiwa ni pamoja na kutambuliwa na Shirika la Afya la Dunia (WHO).
“Uwezo wetu umekuwa mkubwa na tuko karibu na maeneo yote ya udhibiti. Hivi sasa mbali ya ofisi zetu za kanda, lakini pia tuna wawakilishi katika kila Halmashauri nchini,” alisema.
Alifafanua kuwa Halmashauri zote zina wataalamu ambao wanafanya kazi kwa niaba ya Mamlaka ambapo wanasimamia na kudhibiti ubora na usalama wa dawa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa maelekezo ya TFDA.
Hivi sasa TFDA ina ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini na ya Nyanda za Juu Kusini.
Mkurugenzi Mkuu huyo aliwapongeza wataalamu wa taasisi yake kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwashukuru wadau mbali mbali kwa ushirikiano wao na hasa wananchi ambao amesema wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na taasisi yake kutoa taarifa zinazohusu uvunjifu wa sheria.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, katika kipindi cha mwaka 2003 hadi Juni, 2017, TFDA imesajili dawa 12,474.
Kwa upande wa dawa zilizoingizwa na kugundulika kuwa hazina ubora, katika kipindi hicho, TFDA iliteketeza dawa zenye jumla ya thamani Shilingi bilioni 11.591.
Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
No comments