Wazee Chadema wamwomba Rais Magufuli akutane nao
Wakati leo Jumapili dunia ikiadhimisha siku ya wazee, Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limemwomba Rais John Magufuli kukutana na wazee nchini ili kujadiliana na kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali.
Wito huo umetolewa leo na katibu mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka wakati akizungumza na waandishi wa habari makao mkuu wa Chadema jijini Dar es Salaam kuhusu siku ya wazee duniani.
"Wazee ambao tunashauri Rais Magufuli akutane nao ni wazee kutoka vyama vya siasa, viongozi wastaafu wa dini, wastaafu serikalini na awe tayari kupokea ukosoaji wao na kuufanyia kazi," amesema Lutembeka.
Amesema mchakato wa Katiba uliokwama unapaswa kupatiwa ufumbuzi ili kuleta tija kwa Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
"Umuhimu wa Taifa kuwa na Katiba mpya unazidi kuonekana kila siku...Watanzania wanataka Katiba mpya kwa ajili ya kutibu majeraha ya Taifa hili," amesema.
Kuhusu wazee, Lutembeka amesema wamekuwa hawathaminiwi na kutambulika katika ngazi za uamuzi, afya na ndani ya jamii.
Amesema ni wakati sasa kwa Serikali kupeleka muswada wa sheria ya wazee bungeni ili kutekeleza Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003.
Lutembeka amesema kama Serikali haitafanya hivyo, wawakilishi wa wananchi ambao ni wabunge watumie kanuni ya Bunge kuwasilisha muswada binafsi kuhusu sheria ya wazee nchini.
No comments