Dk Slaa amshukuru Mungu kwa Kuteuliwa Kuwa Balozi
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo, Dkt. Wilbroad Peter Slaa, amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua kuwa Balozi wa Tanzania na kusema kuwa yuko tayari kutoa mchango wake katika kulijenga taifa la Tanzania.
“Kwa sababu Ubalozi uko kwenye Idara za moja kwa moja za mkuu wa nchi, na bila shaka hakukuwa na sababu mkuu wangu kutotaka kuniteua, ninamshukuru kwa uteuzi huo kwa kuniona, ninachoweza tu kusema katika hatua hiyo ni kwamba ninao wajibu mkubwa hasa katika kipindi hichi cha kulijenga taifa letu,” amesema Dkt. Slaa.
Dkt. Slaa ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, na ambaye aliwahi kugombea nafasi ya Urasi kupitia chama hicho, alijiuzulu nafasi yake hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuondoka nchini.
Muda mfupi baadaye Dkt. Slaa alitangaza kutojihusisha tena na siasa za hapa nchini na akawa anaishi nchini Canada pamoja na mpenzi wake Josephine Mushumbusi.
Dk. Slaa, ambaye kwa sasa anaishi nchini Canada alikokwenda kwa masomo, tangu alipotangaza kuachana na siasa Septemba 1, mwaka 2015 aliweka wazi kuwa anafanya kazi zaidi ya mbili ili aweze kujipatia kipato kitakachomuwezesha kumudu gharama za maisha nchini humo.
Alitaja kuwa kwa sasa anafanya kazi ya Mshauri wa Mauzo (sales Advisor) pamoja na kutoa ushauri (consultancy).
“Mimi ninafanya kazi PWD/CDS/COSTCO kama Sales Advisor, baada ya kumaliza masomo yangu hasa Interpersonal Communication. Costco ninakofanya kazi ina members (wanachama) 10,000. Kwa siku wanaofika Warehouse ni kati ya 5,000 hadi 7,000,” alisema Dk. Slaa.
Kufuatia uteuzi huo wa Dkt. Slaa kuwa Balozi uliofanywa na Rais Magufuli, taaarifa kutoka ikulu imeeleza kuwa zoezi la kuapishwa kwake litafuata baada ya kukamilishwa kwa taratibu.
No comments