Breaking News

Mkurugenzi ashindwa kutoa takwimu mbele ya Rais


Rais John Magufuli amewabana wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na Manispaa ya Bukoba akitaka kujua matumizi ya fedha za mfuko wa barabara zilizopelekwa huku baadhi ya viongozi wakishindwa kutoa majibu.

Akizungumza leo  Novemba 6 ,2017 wakati wa uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba, Mkoani Kagera Rais Magufuli amesema anashangazwa kuona viongozi aliowateua wanakosa majibu juu ya fedha za Serikali.

Kama ilivyo ada, Rais Magufuli ameanza kwa kuwaeleza wananchi juu ya mabadiliko aliyoyafanya tangu aingie madarakani ikiwamo udhibiti wa watumishi hewa na vyeti feki akisema mambo hayo yameigharimu nchi.

Baada ya kuzungumza masuala hayo aliwaita viongozi wa halmashauri ya Bukoba kwenye mkoa huo akitaka kueleza ni kiasi gani cha fedha za mfuko wa barabara walizopokea pamoja na matumizi yake.

“Serikali huwa inaleta fedha kwaajili ya maendeleo ya kila manispaa na hata hapa tumeshaleta,”

“Mkurugenzi wa Manispaa,tumeleta kiasi gani hapa? bajeti ya manispaa ya Bukoba ni kiasi gani?amehoji na kwamba anataka watu wajue matumizi yake.

Mkurugenzi wa manispaa hiyo Erasto Mfugale , amemueleza kuwa hadi sasa amepokea Sh33 bilioni ikiwa ni bajeti ya jumla huku akishindwa kutolea majibu fedha za mfuko wa barabara.

 “Katika fedha hizo kuna fedha ambazo ni mishahara ambazo ni mishahara Sh19 bilioni kwa mwaka,”amesema

Kabla hajamaliza, Rais alimuuliza “fedha za road fund (mfuko wa barabara)ni kiasi gani, nasema hivi kwasababu zinapoteaga poteaga tu nataka uziseme hapahapa,”amesisitiza

Mkurugenzi huyo ameshindwa kutoa majibu suala ambalo rais ameliita ni kucheza na fedha za Serikali.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri, Mwantum Dau alivyosimama kutoa majibu alisema hakumbuki ni kiasi gani suala ambalo limeonekana kumkasirisha rais.

“Hapana mheshimiwa Rais labda aje mtunza hazina, mimi nina idara nyingi siwezi kukumbuka,” alisema

Rais amesema anashangaa kuona viongozi aliwateua hawajui kuhusu fedha za Serikali.

“Nani anafahamu hela za mfuko wa barabara manispaa ya Bukoba kwa sababu viongozi niliowateua hawajui,pengine naweza nikateua Mkurugenzi sasa hivi,”amesema

Meya wa Manispaa hiyo  Jerry Silaa  ndiye aliyewanasua viongozi hao baada ya kueleza jumla ya fedha Shmilioni700 za ujenzi wa barabara pamoja na Sh120 kwaajili ya maboresho.

No comments