Polisi Watumia Mabomu ya Machozi Kuwatawanya Wafuasi wa Lowassa
Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wamelazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi kumwezesha mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kupata nafasi ya kupita mjini Moshi.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walitumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wamefunga barabara.
Takriban mabomu manne ya kutoa machozi yalifyatuliwa saa 10:30 jana jioni ya Jumamosi Novemba 18,2017 katika eneo la Soko la Manyema ambako Lowassa na msafara wake alikuwa apokewe ili kuelekea kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za udiwani eneo la Pasua Relini.
Kabla ya Lowassa kufika, vijana madereva wa bodaboda walipita katika Barabara ya J.K. Nyerere.
Vijana hao walipopita mzunguko wa magari wa Coca Cola saa 10:15 jioni, gari la polisi aina ya Toyota Land Cruicer likiwa na polisi wenye mabomu ya machozi lilionekana likiwafuata.
Haikupita dakika 15, ndipo kulisikika milio ya mabomu katika eneo la Manyema ambalo ni njia panda ya kuelekea eneo la mkutano.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema ambaye yuko katika msafara wa Lowassa, alisema eneo la Manyema lilikuwa halipitiki kutokana umati wa watu.
Lema alisema ni kutokana na hali hiyo, ili kumwezesha Lowassa na msafara wake kupita, FFU walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mabomu hayo yamepigwa ili kupunguza idadi ya watu waliokuwa wamefurika kwenye eneo hilo na kumuwezesha Lowassa kupita.
“Alikuwa hana njia ya kupita, watu walifurika kiasi kwamba hata Lowassa mwenyewe asingeweza kupita, tulifanya hivyo kuwapunguza na ameshapita ameenda zake kwenye mkutano,” alisema.
No comments