Breaking News

Waziri aagiza uchunguzi wa aliyetoa stika kwa basi bovu



Serikali imeagiza kufanyika uchunguzi wa askari mkoani Tabora aliyekagua na kutoa stika ya usalama barabarani kwa basi la abiria mali ya kampuni ya Mtoto Gema ambalo limebainika kuwa bovu.

Basi hilo limebainika kuwa na hitilafu katika mfumo wa usukani leo Jumapili Novemba 5,2017 mjini Dodoma lilipokaguliwa katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani.

Agizo la kufanyika uchunguzi kwa askari waliohusika kutoa stika hiyo, limetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliyefika kituoni kuangalia ukaguzi wa lazima wa magari.

“Tulikubaliana kila mkoa uandae maeneo maalumu ya ukaguzi wa magari ya abiria, mizigo na ya wanafunzi. Pia, yakaguliwe ipasavyo kabla ya kutoa stika. Kwa hiyo, leo nimekuja kuangalia utekelezaji wa maagizo hayo,” amesema.

Masauni amesema licha ya wamiliki kutoitikia wito wa kupeleka magari kukaguliwa, wamegundua changamoto nyingine ni baadhi yao na askari kutekeleza majukumu yao kwa mazoea.

Amesema sasa wanatoa mwaka mmoja kwa ukaguzi wa lazima wa magari lakini wanafikiria kupunguza muda huo ili kufanyika mwingine.

“Gari limepewa stika wiki mbili limezuiwa hapa kwa ubovu, inaonekana ni uzembe wa hali ya juu ambao ulifanywa na ofisa wetu ambaye ametoa stika Tabora,” amesema Masauni.

Amesema, “Hatutaliacha hili lipite hivihivi, nilishaagiza nipatiwe taarifa ya kina kuhusu hili, tutalichunguza na tutamchukulia hatua kali yule ambaye ameshiriki kwa namna yoyote ile ili iwe fundisho kwa Wengine.”

Masauni ametoa agizo kwa maofisa wote wanaohusika na ukaguzi wasipotekeleza majukumu yao kwa sababu yoyote ikiwemo rushwa au uzembe watashughulikiwa.

Wakala wa kampuni ya Mtoto Gema mjini Dodoma, Frank Lukumay amesema basi hilo lilikaguliwa Tabora na kupewa stika ya usalama barabarani lakini katika ukaguzi wa kawaida leo wamebaini hapakuwa na mafuta katika mfumo wa usukani.

Mkuu wa Ukaguzi wa Magari na Mtahini katika Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dodoma, Erasmus Russa amesema tangu ukaguzi uanze wamebaini mabasi ya abiria 62 kuwa mabovu ambayo yamezuiwa kufanya kazi.

Amesema mabasi 10 kati ya hayo yametengenezwa na kurejeshwa kwa ukaguzi na mengine hayajarejeshwa.

Kuhusu magari ya kubeba wanafunzi, amesema ni shule tano pekee zilizoyapeleka kwa ukaguzi

No comments