Breaking News

Waziri Mkuu awataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri na Naibu Mawaziri wajiepushe na utoaji wa matamko yasiyotekelezeka ili kuepuka mikanganyiko Serikalini.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Novemba 7, 2017) wakati akifungua Kikao Kazi cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema ni vema  viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za wizara zao.

Pia amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais Dkt. John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.

“Tunao wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli na wananchi wote kwa ujumla.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za Wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.

Pia amewataka wafanye ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Waziri Mkuu amesema Mawaziri na Naibu Mawaziri wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.

 Pia wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt. Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.

No comments