Zitto Kabwe Akerwa na Biashara ya Watumwa Inayoendelea Libya.....Aitaka Tanzania isiingie Uwanjani dhidi ya Libya Jumapili
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe ameitaka timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kutoshuka dimbani kuikabili Libya siku ya Jumapili katika michuano ya CECAFA ikiwa ni hatua ya kuonyesha kuchukizwa na vitendo vya biashara ya utumwa vinavyoendelea katika nchi hiyo.
Zitto ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter ikiwa zimesalia siku chache kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara kucheza mchezo wake wa kwanza siku ya Jumapili ya Desemba 3 dhidi ya Libya katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati inayofanyika huko nchini Kenya.
Leo @masoudkipanya ameshauri Tanzania isusie mechi yake dhidi ya Libya siku ya Jumapili kuonyesha kuchukizwa na Biashara ya Utumwa. Ninaunga mkono. Tanzania isiingie Uwanjani kucheza na Libya. @SADC_News iagize nchi zake zote zirudishe mabalozi wake kutoka Libya.
Kilimanjaro Stars itacheza mchezo huo wa kundi A, katika kuwania kombe la michuano ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA ambayo inatarajiwa kuchezwa nchini Kenya kuanzia Desembe 3 hadi 17 mwaka huu.
Mataifa 10 yanatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo mikubwa kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki huku droo ya hatua ya makundi ikionyesha mwenyeji Kenya itacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Rwanda huku Tanzania ikiikabili Libya siku hiyo.
No comments