Breaking News

Serikali kuajiri waalimu wa shule za msingi na sekondari


Serikali imepanga kuajiri walimu 11,000 wa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha wa 2017/18.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo alisema katika mpango huo, walimu 7, 000 watakuwa wa shule za msingi na 4,000 wa sekondari.

“Hadi kufikia Desemba 31, walimu 2,700 watakuwa wameshaajiriwa,” alisema Jaffo

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati wa kurekodi kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kurushwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari, Jafo alisema ajira hizo zitapunguza upungufu wa walimu unaotokana na ongezeko la wanafunzi tangu Sera ya Elimu Bure ya Msingi ianze kutekelezwa.

Tangu mwaka jana, Serikali inatekeleza sera hiyo inayoligharimu Taifa zaidi ya Sh20 bilioni kila mwezi, huku idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi na wale wanaojiunga na za sekondari ikiongezeka kwa zaidi ya wanafunzi milioni moja.

Kuhusu miundombinu shuleni alisema kwamba Serikali imetenga zaidi ya Sh37 bilioni za ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari za umma 148.

Akifafanua, Jafo alisema zaidi ya Sh21 bilioni zimetumika kujenga mabweni 85 katika awamu ya kwanza ya mpango huo, huku awamu ya pili ya kujenga mabweni 65 iliyoanza kutekelezwa Agosti ikitarajiwa kugharimu Sh16 bilioni.

Kuhusu matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa, Waziri Jafo alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh246 bilioni kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa katika shule za umma.

“Theluthi moja ya fedha hizo, sawa na Sh82 bilioni zitatumika kukamilisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi,” alisema.

Waziri Jafo alisema kuwa Serikali imepanga kujenga vituo vya afya 172 kwa fedha kutoka Benki ya Dunia (WB), Serikali ya Canada na wadau wengine kupitia mfuko wa pamoja wa kuendeleza Sekta ya Afya (Basket Fund).

“Lengo ni kutekeleza sera ya zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za afya,” alisema Jafo.

Alifafanua kuwa hivi sasa ni kata 530 pekee kati ya 3,900 zilizopo nchini ndizo zenye vituo vya afya.

Kuhusu upatikanaji wa dawa na vifaatiba, alisema Serikali imeongeza bajeti hadi kufikia Sh269 bilioni kwa ajili hiyo.

“Tunazo pia zaidi ya Sh127 bilioni za Basket Fund zitakazoelekezwa kwenye utatuzi wa changamoto ya upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma,” alisema.

Akizungumzia upungufu wa watumishi katika sekta ya afya iliyochangiwa na uhakiki wa vyeti feki, Waziri Jafo alisema tayari Serikali imeajiri watumishi 2,058 huku wengine zaidi wakitarajiwa kuajiriwa.

Suala la uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali mwaka jana liliwanasa zaidi ya watumishi 19, 000 ambao ajira zao zilisitishwa, huku sekta ya afya na elimu zikiathirika zaidi.

No comments