Mamia ya wananchi Iran Waandamana kulaani kuangushwa ndege ya abiria Ya Ukraine
Maandamano makubwa yameripotiwa usiku wa Jumamosi kwenye maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Iran Tehran, baada ya nchi hiyo kukiri kuwa kombora la kijeshi liliiangusha ndege ya abiria ya Ukraine.
Mamia ya watu wameshiriki maandamano hayo ya usiku kuikosoa serikali ya nchi hiyo na hatua yake ya hapo kabla ya kupinga madai kuwa kombora lilikuwa chanzo cha ajali hiyo.
Kulingana na shirika la habari la Isna waandamanaji nje ya chuo kikuu cha Amir Kabir wametaka wote waliohusika na kuangushwa ndege hiyo wajiuzulu..
Wakati huo huo rais Donald Trump wa Marekani ameionya Iran dhidi ya kujaribu kufanya ukandamizaji wa maandamano hayo na kutoa wito kwa nchi hiyo kuruhusu makundi ya haki za kirai kufuatilia kile kinachoendelea.
Ujumbe wa Trump umekuja baada ya polisi kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakitoa kauli kali kuwakumbuka wahanga wa ajali ya ndege iliyotokea Jumatano iliyopita.
No comments