Breaking News

Naibu Waziri wa Madini Ladslausi Nyongo Ataka Wafanyabiashara Wa Madini Wasikamatwe Kamatwe Hovyo

Na Ahmed Mahmoud,Arusha
NAIBU Waziri wa Madini Ladslausi Nyongo  amepiga marufuku tabia ya  kamatakamata ya   wafanyabiashara wa madini nchini waliohifadhi  madini maeneo  wanayotaka kwa mujibu wa sheria.
 
Aidha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 Mkoa wa Arusha umekusanya  zaidi ya Sh.bilioni  30 zinazotokana na madini ya Vito ya aina mbalimbali.
 
Akizungumza jana Jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa Mabalozi wa China nchini Tanzania na Tanzania nchini China pamoja na wafanyabiashara wa madini nchini,Naibu Waziri Nyongo alisema sheria inaruhusu wafanyabiashara kukaa na madini ili mradi wafuate sheria.
 
“Lakini siku za karibuni kumezuka tabia ya kusumbua wafanyabiashara waliofuata sheria za kukaa na  madini kwa kulipa kodi zote wanazotakiwa ili wakauze mahali popote wanapotaka,lakini wanasumbuliwa kwa kukamatwa na vyombo vya ulinzi,”alisema.
 
Alisema ili kuondoa mkanganyiko huo Wizara imejipanga kuelemisha wadau wa madini vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu sheria za madini ikiwemo inayoruhusu wafanyabiashara hao kushikilia madini kabla ya kuuza kwenye soko za madini zilizopo.
 
Aidha aliomba Mabalozi wa China nchini Tanzania na yule wa Tanzania nchini China kuja kuwekeza nchini kwenye uwekezaji wa uongezaji thamani masini chini ya Gramu mbili ambayo yanaruhusiwa kwenda nje ya  nchi bila kuonhezwa thamani.
 
“Kama mnateknolojia ya kuongeza thamani madini haya tunawaalika mje kuwekeza ili tusiyatoe nje bila kuongeza thamani,”alisema.
 
Mkuu wa Mkoa Arusha Mrisho Gambo alisema wameleta mkutano huo ili kuongeza fursa kwa wafanyabiashara katika kupanua wigo wa soko la madini.
 
Alisema nchi ya Tanzania ina madini mengi lakini mchango wake kwa pato la Taifa ni asilimia 5.07 tofauti na pato la sekta ya utalii asilimia  17 na asilimia 25 katika kuingizia Taifa fedha za kigeni.
 
“Mchango huu hautoshi hivyo tumeamua kutumia mkutano huu ili tuongeze fursa katika madini na kukuza zaidi pato la sekta hii,”alisema.
 
Kuhusu ukusanyaji wa madini alisema yanatokana na soko la madini Namanga kukusanya Sh.bilioni 1.7  ya  madini ya vito na soko la Arusha walikusanya Sh.bilioni 34.46 katika kipindi cha Juni 2019 hadi Desemba 2019.
 
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof.Idrisa Kikula aliomba  Ofisa Madini Mkazi wa Mikoa yote kukaa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuelimishana sheria za madini ili wafahamu jinsi ya kudhibiti utoroshaji wa madini.
 
Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki aliomba wafanyabiashara kutumia fursa ya mkutano huo kuongeza mapato ya madini kutoka Sh.bilioni 500 ya sasa hadi kufikia Sh.Trioni moja.
 
“China wanunuzi wakubwa wa dhahabu  kama mwaka jana 2019 walinunua dhahabu tani 1506 hiki sio kiwango kidogo na hata madini mengine wananunua sana hivyo tujitahidi kuongeza fursa za soko nchini China,”alisema.

No comments