Mwigulu Nchemba Atoa Suluhu ya "Watu Wasiojulikana"
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema kutengeneza mioyo yenye maadili mema kwa wazazi, watoto na jamii kwa ujumla ni miongoni mwa suluhisho la kudumu la jamii kutokuwa na watu wasiojulikana.
Nchemba ameitoa kauli hiyo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 57 ya Ushirika wa Wanafunzi wa Kiinjili wa Tanzania (Tafes) yaliyokwenda sambamba na kusherehekea miaka 27 ya uwepo wao hapa nchini.
Tafes ni taasisi isiyo kiserikali inayojishughulisha na kuwajengea uwezo wa kiroho wanafunzi wa vyuo vikuu ili wawe na misingi bora ya uongozi katika ngazi mbalimbali.
Amesema maandalizi ya maadili mema yaanza katika ngazi ya familia na taasisi za kiroho na kwamba, Serikali inawaandaa watu kwa shule, kiafya, lakini afya na uaminifu wa kiroho utatoka kwenye taasisi hizo.
Nchemba ambaye pia Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), amesema uhalifu wa kikatili ni zao la kutokuwapo kwa hofu ya Mungu kwenye mioyo ya watekelezaji wa matukio ya aina hiyo.
"Labda niwaambieni kuna watu wana roho mbaya na wengi wana uwezo kufanya vitu vibaya. Wakati Serikali tunashughulikia jambo hilo, tunazipongeza jitihada kama hizi zinazolenga kubadilisha jamii nzima inayofanywa na Tafes," amesema Nchemba.
Alisema watu wa vyuo vikuu wana famalia zao na kwamba wakiwa maadili mema itawasaidia kuwaelimisha jamii zinazowazunguka kuhusu misingi bora ya maadili.
"Tukiwa na watu waliolelewa katika misingi ya imani ya aina hii, hatuwezi tukapata watu wasiojulikana na jambo hili linaniudhi sana. Hatuwezi tukawa na watu wasiojulikana, wanaotenda uhalifu na kukimbia kusikojulikana na tutashughulika na nguvu ya dola," amesema Nchemba.
Mbali na hilo, Mwigulu ameongeza kwamba Tafes kwa kazi wanayoifanya huku akitumia msemo wa nahau ya' Usione vyaelea ujue vimeundwa'.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Bodi ya Tafes, Profesa Lazaro Busagala amesema lengo la taasisi hiyo ni kuwatengeneza na kuwajengea uwezo wanafunzi wa vyuo vikuu wa kuwa na maadili mema.
Alisema wametumia nafasi ya maadhimisho hayo kupeana moyo namna ya kuwasaidia kiroho na kimaadili wanafunzi wa vyuo vikuu ili baadaye wasiwe viongozi wazembe na wala rushwa.
"Hadi sasa Tafes imeweza kuwafikia wanafunzi 5000 wa vyuo vikuu mbalimbali," amesema Profesa Busagala.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya hafla hiyo, Dk Grace Kazoba amesema walitumia maadhimisho hayo kuweka msisitizo wa misingi bora itakayowasaidia wanafunzi hao.
No comments