Breaking News

Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi ajali ya Uganda


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi aliyewahi kuwa Naibu Waziri na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mpwapwa Mkoani Dodoma Bw. Gregory Teu kufuatia vifo vya watu 13 ambao ni ndugu wa familia yake waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea nchini Uganda. Watu hao wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana na lori tarehe 17 Septemba, 2017 majira ya saa 4:00 Usiku katika barabara ya Masaka nchini Uganda wakiwa njiani kurejea Tanzania. “Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa ya watu, nampa pole Ndg. Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa, nawapa pole wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi. “Nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote wanaopata matibabu huko nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani” amesema Mhe. Rais Magufuli. Mhe. Rais Magufuli amewataka wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea. Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU Dar es Salaam 18 Septemba, 2017

No comments