Babu Seya na Papii Kocha Baada ya Kuachiwa Huru Jana Jioni
Mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ wametoka katika gereza la Ukonga jana jioni baada ya kusota kwa miaka 13.
Wanamuziki hao ‘baba na mwana’ walitoka katika kifungo cha maisha baada ya kupata msamaha wa Rais John Magufuli jana Jumamosi Desemba 9, mwaka 2017.
JPM alitoa msamaha kwa baadhi ya wafungwa alipokuwa akihutubia Taifa kusherehea miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miongoni mwa waliopata ahueni hiyo ni Babu Seya na Papii Kocha.
“Babu, babu, babu,” zilikuwa ni kelele za mashabiki na ndugu zake waliompokea Babu Seya na Papii Kocha waliokuwa wametoka gerezani wakiwa na magitaa yao mgongoni.
Babu Seya aliyeonekana mtanashati alionekana anapunga mkono wa kulia kama mtu asiyeamini huku Papii Kocha akipunga mkono akionekana kufurahia na kuzungumza na mashabiki.
Walisindikizwa na askari magereza mpaka nje na kulikuwa na foleni kubwa kutokana na tukio hilo.
No comments