Breaking News

Chadema wadai Rais Magufuli ametekeleza ahadi ya Lowassa Kumwachia Babu Seya


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimempongeza Rais John Magufuli kwa kutekeleza ahadi zilizotolewa na mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa ikiwemo ya kuwaachia huru wanamuziki Nguza Viking na Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.

Taarifa iliyotolewa jana  Jumamosi na chama hicho ilieleza kuwa katika ahadi zake Lowassa aliahidi iwapo Chadema ingeshinda uchaguzi angewaachia wanamuziki hao.

Vilevile chama hicho  kimetoa wito kwa  Serikali kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa sheria kuondoa nia ya kuwashtaki masheikh wa Zanzibar na mahabusu na washtakiwa wa makosa ya mtandao.

==>Hii ndo kauli ya CHADEMA
Tunampongeza Rais John Pombe Magufuli kwa ujasiri wa kuendelea kutekeleza baadhi ya ahadi zilizotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa Mgombea wa Urais, Mhe. Edward Lowassa, wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, ambapo leo akihutubia sherehe za siku ya Uhuru wa Tanganyika, ametoa msamaha kwa waliokuwa wafungwa wa kifungo cha maisha, Ndugu Nguza Vicking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha).

Kutokana na kitendo alichofanya leo Rais Magufuli kwa kutumia ibara ya 45 ya Katiba ya Nchi, kama ambavyo mgombea wetu wa urais aliahidi iwapo CHADEMA ingeshinda uchaguzi, kushika dola na kuongoza Serikali, Chama kinatoa wito kwa Serikali itumie mamlaka yake kwa mujibu wa sheria za nchi, hususan kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa utaratibu wa *Nolle Prosqui*, iondoe nia ya kuendelea kuwashtaki;

1. Masheikh wa Zanzibar wanaoshtakiwa Mahakama ya Kisutu, Tanzania Bara.

2. Mahabusu na watuhumiwa wa makosa ya mitandao.

3. Watuhumiwa na mahabusu wa makosa ya kisiasa, ikiwemo kesi za uchochezi, zinazohusisha kumkosoa Rais Magufuli, kuikosoa Serikali yake na chama chake au tuhuma zinazotokana na kutekeleza shughuli halali za kisiasa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi, ikiwemo maandamano, mikutano ya hadhara na vikao vya ndani.

Imetolewa  Jumamosi, Desemba 9, 2017 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments